Dar es Salaam. Sio kila homa ni Malaria, nenda ukapime. Bila shaka maneno haya sio mageni kwa watanzania wengi kwani yamewahi kuwa wimbo wa kampeni ya kitaifa katika kuwahimiza watu wasiwe na tabia ya aidha kwenda kujinunulia dawa kwenye duka la dawa bila kwenda kwa daktari, na hivyo kutibu ugonjwa ambao pengine sio ambao wanaumwa na wanaopaswa kuutibu. Ukisikia kichwa kinauma, au tumbo, mwili kuchoka, kukosa hamu ya kula, au namna fulani ambayo pengine huwa inakutokea unapopatwa na Malaria, unafanya nini? Tafiti zinaonyesha kuwa, watu wengi huamua kwenda duka la dawa kununua dawa ya Malaria kabla ya kwenda hospitali. Hali hii ni ya hatari, hasa ukizingatia kuwa Malaria ni moja ya magonjwa makuu matano yanayosababisha vifo vya watu wazima Tanzania (asilimia 7).
Na unaweza kufahamu kituo cha afya kilichopo karibu nawe kwa nyezo kama hii iliyotengenezwa na shirika la Code4Africa. Hata hivyo, utafiti ulioangalia jinsi watu wanavyojitibu, uliochapishwa mwaka 2014 unaonyesha kuwa watu wengi hufanya hivyo endapo kuna uhaba wa dawa kwenye vituo vya afya, au kuna foleni kubwa kwenda kumuona daktari, au kituo cha afya kiko mbali, au hana uwezo wa kifedha kulipia huduma za afya kwenze kituo cha afya, au anaona bora awe na uhuru wa kuchagua dawa anayotaka mwenyewe. Hivyo, ipo haja ya kuboresha huduma za afya ili wagonjwa wapate urahisi wa kutibiwa, na kuvutiwa zaidi kupata ushauri wa mtaalamu kwanza kabla ya kufanya maamuzi ya kutumia dawa wao wenyewe.
Katika utafiti uliofanywa na Young Initiatives Tanzania (YITA) kwa kushirikiana na shirika la Twaweza (mwaka 2011), Ununuzi wa dawa Tanzania, ilibainika kuwa katika ziara 88 zilizofanywa katika maduka ya dawa, watafiti waliingia dukani na moja kwa moja kuulizia kununua aina fulani ya dawa inayohitaji mteja aonyeshe agizo la dawa lililoandikwa na daktari bila kuonyesha agizo hilo. Katika ziara 82 kati ya ziara za aina hiyo (asilimia 93), wahudumu waliuza dawa zilizotakiwa na wateja bila kuulizia agizo la daktari.
Katika ziara 38 watafiti waliomba ushauri kutoka kwa wahudumu baada ya kuzungumza nao juu ya ugonjwa na/au dalili ya ugonjwa huo. Katika ziara 35 kati ya ziara hizo 38 (asilimia 92), baada ya mhudumu kumshauri mgonjwa akamwone daktari kwanza, mhudumu alimshauri mteja anunue dawa ya aina fulani, ambzo zingepaswa kutolewa tu baada ya kuonyesha agizo la dawa lililoandikwa na daktari, na kumuuzia dawa hizo.
Kwa ujumla, ziara 117 kati ya 126 (asilimia 93), dawa zilizohitaji mteja kuwa na agizo la dawa kutoka kwa daktari ziliuzwa bila mhudumu dukani kuulizia agizo hilo. Ni mara tisa tu (asilimia 7) ambapo wateja walikataliwa kuuziwa dawa kwa kushindwa kuonyesha agizo la daktari.
Ripoti inaonyesha kuwa kwa ujumla, ilikuwa rahisi kupata dawa zinazohitaji agizo la dawa kutoka kwa daktari karibu katika nyakati zote, isipokuwa katika maeneo machache tu. katika maeneo 12 kati ya 15 yaliyotembelewa, watafiti waliweza kupata dawa hizo bila kuonyesha agizo la dawa lililoandikwa na daktari katika asilimia 100 ya ziara walizofanya.
Takwimu zinaonyesha kuwa Malaria ni moja ya magonjwa makuu matano yanayosababisha vifo Tanzania. Ripoti ya TDHS-Malaria (2015-16), inaonesha kuwa kuenea kwa ugonjwa wa Malaria kumeongezeaka kutoka asilimia 9 katika kipindi cha mwaka 2011-12 hadi asilimia 15 mwaka 2015-16. Malaria bado inaendela kuwa ugonjwa unaosababisha idadi kubwa ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano kulazwa, kwenda kwenye vituo vya afya kwaajili ya matibabu, na pia kama sababu ya kifo.
Utafiti ulioangalia jinsi watu wanavyo “jitibu”, unaonyesha kuwa kwa kiwango kikubwa, hali hii ni ya kawaida kwa watu waishio katika ulimwengu unaoendelea. Hii inatokana na kushindwa kumudu gharama kubwa za matibabu na huduma za afya kiujumla. Hivyo watu hutumia mitishamba, dawa za kienyeji, au kununua dawa kwenye dula la dawa bila kuwa na maelekezo yoyote ya daktari ya jinsi ya kutumia dawa hizo.
Kwa upande wa watoto, ripoti ya TDHS-Malaria 2015-16 inaonyesha kwamba kiwango cha elimu cha mama, pamoja na uwezo wake kiuchumi, unachangia sana namna ambavyo anamjali mwanae apatapo homa. Mama akiwa na kiwango kikubwa cha elimu na fedha, kuna uwezekano mkubwa zaidi kwamba mtoto atapewa antibiotiki. Hata hivyo, ni kimyume kwa dawa za malaria. Kama mama ni msomi na mwenye kipato kizuri, atasita kumpa mwanae dawa za Malaria bila kwenda kwa mtaalamu wa afya.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa watoto wenye umri wa kati ya miezi 6 na 35 hupata homa zaidi ya wale wenye umri chini za miezi 6 au wale wenye umri zaidi ya miezi 35. Huku kiwango cha watoto wanaopelekwa kwenye vituo vya afya kabla ya kupewa dawa ikiwa tofauti kulingana na mnapoishi. Kwa wanaoishi mijini, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kupata ushauri wa daktari kwanza. Ambapo watoto saba kati ya kumi (asilimia 69) hutafuta ushauri wa mtaalamu kwanza kabla ya kumeza dawa. Kwa wanaoishi vijijini, ni asilimia 43 tu hutafuta ushauri wa mtaalamu kwanza.
Moja ya hatari ya kutumia dawa za Malaria bila kuandikiwa na daktari, ni kupata sugu ya dawa. Hii huweza kupelekea, mtu kutibu ugonjwa ambao hana. Hivyo wataalamu wanashauri kuwa ipo haja ya kutoa elimu kwa wananchi, hasa wanaoishi vijijini, pamoja na wahudumu wa afya, kuhusu matumizi sahihi ya dawa na utaratibu unaopaswa kufuatwa kabla ya kutumia dawa. Wananchi pia wanayo fursa ya kutumia nyenzo iliyobuniwa na Code4Africa kuhakiki dawa wanazotaka kutumia.
Dawa ya ARV je?
Dawa za kufubaza makali ya maambukizi ya virusi vya ukimwi (vvu), ARV husambazwa na serikali, kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali wa sekta ya afya. Tukiangalia mkoa wa Mbeya, ambao ni mkoa wa pili kitaifa katika maambuki mengi ya vvu, wataalamu wa huduma za afya wanasema kuwa dawa za ARV zinawafikia walengwa kwa asilimia 95 hadi 100. Mkoa unaoongoza kitaifa ni Njombe. Meneja Bohari ya Dawa Kanda ya Mbeya ananukuliwa akisema kuwa kwakuwa kuna uhitaji mkubwa wa dawa hizi, serikali inahakikisha kuwa upatikanaji wake ni wa urahisi.
Matokeo ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya Ukimwi nchini wa mwaka 2016/17 yanaonesha kuwa kuwa zaidi ya nusu (asilimia 52) ya watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64 wanaoishi na vvu nchini vipimo vinaonyesha kuwa kiasi cha virusi mwilini kimefubazwa. Takwimu zinaonesha kuwa mkoa wa Mbeya uko kati ya mikoa kumi inayofanya vizuri, ambapo asilimia 57.4 ya watu wote wenye vvu, virusi vyao vimefubazwa.
Leave a Reply