Dar es Salaam. Kumekuwa na jitihada nyingi za serikali na wadau mbalimbali kuboresha miundombinu ya afya na kuwahamasisha akina mama kujifungua katika vituo vya matibabu ili kupunguza vifo vya akina mama na watoto vitokanavyo na uzazi. Hili ni moja ya malengo 17 ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa ambayo yanatarajiwa kufikiwa mnamo mwaka 2030, yaani kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi hadi kufikia uwiano wa 70 kwa vizazi hai 100,000.
Kuna idadi kubwa ya vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi nchini. Ripoti ya jamii na afya ya ofisi ya Taifa ya Takwimu, 2015-16 TDHS-MIS yaonyesha kuwa kuna vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000. Idadi ambayo bado ni kubwa. Hata hivyo, jitihada za kuwahamaisha wanawake wajifungulie kwenye vituo vya matibabu kwa kuongeza elimu na kuboresha huduma, zinaonekana. Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mwaka 2013 na 2014, kulikuwa na ongezeko la asilimia 10 la wanawake wanaojifungulia kwenye vituo vya matibabu na punguzo la asilimia 2 la wanaojifungulia majumbani. Tukichambua zaidi, tunaona kwamba takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2013, idadi ya wanawake waliojifungua kwenye vituo vya matibabu ilikuwa 1,073,348. Kwa mwaka uliofuata idadi hiyo iliongezeka hadi kufikia 1,195,749; ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 10. Kwa upande wa wanawake waliojifungua majumbani, idadi yao ilikuwa 101,917 kwa mwaka 2013. Idadi hiyo ilipungua mwaka 2014 hadi kufikia 98,831; ambayo ni sawa na punguzo la asilimia 2. Zipo jitihada za wadau mbalimbali pia, ikiwemo nyenzo iliyoandaliwa na Code4Africa, ambayo inamsaidia mama mjamzito na jamii inayomzunguka kutafuta mtandaoni kituo cha afya kilichopo karibu yake.
Mikoa mitano inayoongoza kwa wanaojifungua kwenye vituo vya matibabu
Takwimu zinaonyesha kuwa, wanawake wengi hujifungulia kwenye vituo vya matibabu kuliko mahali pengine popote, ambapo zaidi ya wanawake 6 kati ya 10 hujifungua katika vituo vya matibabu. Zaidi ya nusu ( 51%) ya wanaojifungua huenda kwenye vituo vinavyomilikiwa na serikali.
Katika hili, mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na wanawake 128,853 wanaojifungua kwenye vituo vya matibabu (asilimia 10.8). Mwanza, wanawake 79,077 (7%); Mbeya, wanawake 78,732 ( 7 %); Dodoma, wanawake 63,208 ( 5 %); na Tabora, wanawake 61,457 (5%).
Upimaji wa Ukimwi kwa wamama wajawazito katika vituo vya afya
Mkoa wa Mbeya ndio mkoa unaoongoza kwa kuwa na vituo vingi vya kupima virusi vya ukimwi (VVU) na kutoa ushauri nasaha kwa kuwa na jumla ya vituo 317 kati ya 2,672 vilivyopo nchi nzima. Hii ni sawa na asilimia 11.9. Takwimu za programu ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kukabiliana na Ukimwi PEPFAR zilizokusanywa kati ya Oktoba 2014 na Septemba 2015, zinaonesha kuwa asilimia 7 ya wamama wajawazito mkoani Mbeya wana virusi vya ukimwi (VVU). Asilimia 95 ya wamama hao walipewa dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs). Pia, takwimu hizo zinaonyesha kuwa wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ndiyo wilaya yenye wanawake wengi wajawazito wenye vvu, ikifuatiwa na wilaya ya Kyela iliyopo mkoni humo pia.
Ripoti iliyochapishwa na jarida la BMC Pregnancy and Childbirth, uliochapishwa mwaka 2016, unaonyesha kwamba jamii ina mapokeo chanya kuhusu kujifungulia kwenye vituo vya matibabu kwasababu ya kujali usalama wa mama na mtoto. Hali hii inachangiwa na kuongezeka kwa uelewa wa wazazi kuhusu afya ya uzazi; hatua madhubuti kuwaelimisha wanawake wadogo, walioanza uzazi au wenye watoto wengi, juu ya faida za kujifungulia kwenye vituo vya matibabu; wanawake kuona umuhimu wa kujifungulia kwenye vituo vya matibabu baada ya kupata matatizo wakati wa kujifungua hapo nyuma; wanawake kupata matunzo mazuri wakiwa hospitali na hivyo kuhamasishwa kurudi tena; baadhi ya vijiji kukataza wanawake kujifungulia majumbani, na hata kuwatoza faini; ongezeko la vituo vya matibabu pamoja na ongezeko la njia za usafiri wa kuaminika, ikiwemo usafiri wa bodaboda.
Mikoa mitano iliyoongoza kwa wanaojifungua majumbani
Mkoa wa Mara ndio wenye idadi kubwa ya wanaojifungua majumbani. Takwimu zinaonyesha, kwa mwaka 2014, wanawake 10,586 walijifungua nyumbani (10.7%); Kagera, wanawake 9,354 (9.4%); Simiyu, wanawake 8,336 (8.4%); Dar es Salaam, wanawake 7,562 (7.7%); na Mbeya, wanawake 7,171 (7.3%).
Utafiti pia umeonyesha kuwa wanawake waliojifungulia majumbani huwa na nia ya kujifungulia kwenye vituo vya matibabu lakini huishia kujifungulia nyumbani kwa sababu mbalimbali ikiwemo wenza wao kusafiri muda wa kujifungua unapowadia, na kuachwa wenyewe nyumbani. Kuwa nyumbani wenyewe kunachangia kushindwa kulipia usafiri wa kwenda kwenya vituo vya matibabu, kwani mara nyingi wanaume ndio wanaoshughulikia usafiri, ikiwemo kulipia usafiri huo. Cha kushangaza ni kwamba, hata kama mama mjamzito angekuwa ameachiwa pesa na mumewe za usafiri, bado angeona uzito kutafuta usafiri kwa kipindi hicho. Hii inaonyesha kuwa kwa kipindi hiki, kuna uhitaji wa kuwa na mume wake au ndugu wengine wa karibu ili wamsaidie kufanya maamuzi ya haraka.
Kwa wale wanawake ambao waume zao walikuwa nyumbani wakati wanashikwa na uchungu na bado wakaamua kujifungulia nyumbani, huduma isiyoridhisha katika vituo vya matibabu huchangia maamuzi yao.
Tofauti ya mijini na vijijini
Ipo tofauti kati ya wanawake wanaojifungua mjini na vijijini. Ripoti ya TDHS 2015-16 inaonyesha kuwa asilimia 12.8 ya wanawake wanaojifungua mijini hufanya hivyo majumbani, na asilimia 86.4 hujifungua kwenye vituo vya matibabu. Wakati wanawake wa vijijini wanaojifungua majumbani ni kubwa zaidi (44%), na asilimia 53.7 hujifungua kwenye vituo vya matibabu, kwa wanawake wa vijijini.
Pamoja na kwamba idadi ya wanawake wanaojifungua majumbani ni kubwa kwa wanawake walioko vijijini, takwimu zinaonyesha kuwa idadi hiyo imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka.
Ripoti ya Unicef ‘Watoto na Wanawake Tanzania’ (2010), inaonyesha kuwa wanawake wanaojifungua vijijini wako katika wakati mgumu zaidi ukilinganisha na wale walioko mijini bila kujali kama wanajifungua nyumbani au kwenye vituo vya matibabu. Ingawa wanawake wanaojifungua vijijini ni wengi zaidi (asilimia 80 ya wote wanaojifungua), huduma za haraka kwaajili ya akina mama ni duni vijijini. Huku robo ya vituo vya vijijini vikiwa na huduma zote zinazohitajika wakati wa uzazi.
Mikoa mitano yenye idadi kubwa ya wanaojifungua*
Takwimu za mwaka 2014, zinaonyesha kuwa asilimia 10 ya watoto wote wanaozaliwa nchini huzaliwa mkoani Dar es Salaam, ambako kuna wastani wa wanawake 141,098 waliojifungua kwa mwaka, ikifuatiwa na mkoa wa Mbeya ambako kuna waliojifungua 90,823 (asilimia 6.5) na Mwanza waliojifungua 89,749 (asilimia 6). Dodoma ni mkoa wa nne wenye idadi kubwa ya wanaojifungua, ukiwa na jumla ya wanaojifungua 73,381 (asilimia 5); na Tabora una wanaojifungua 71,032 (asilimia 5).
Mikoa mitano yenye idadi ndogo ya wanaojifungua*
Kwa upande mwingine, mikoa yenye idadi ndogo ya wanaojifungua ni mkoa wa Katavi, wenye wanawake 20,491 wanaojifungua ambayo ni sawa na asilimia 1.5 ya wanawake wanaojifungua kwa mwaka nchini nzima. Ikifuatiwa na mkoa wa Njombe wenye wanawake 23,887 wanajifungua (asilimia 1.7); Lindi, wanawake 27131 wanaojifungua (asilimia 1.9); Iringa, wanawake 33651 wanaojifungua (asilimia 2.4), na Mtwara, wanawake 38,264 wanaojifungua (asilimia 2.7).
Leave a Reply