Dar es Salaam. Mariana Hinju (35), anakumbuka jinsi ambavyo alimuuguza mama yake mwaka mmoja uliopita. Hinju, ambaye ni mama wa watoto wanne, alimleta mama yake kutoka Bukoba ili apate huduma nzuri ya matibabu ya macho. “Mama alikuwa na mtoto wa jicho. Ilibidi afanyiwe upasuaji kwenye macho yote mawili. Kwahiyo nikamleta Dar es Salaam ili apate huduma nzuri,” alisema Hinju. Hata hivyo, gharama za matibabu zilikuwa kubwa mno kwani mama yake hakuwa na bima ya afya. Ilibidi amhudumie mama yake kwa kidogo alichokuwa nacho. “Huduma ya upasuaji kwa jicho moja, pamoja na dawa, iligharimu shilingi laki sita. Tulijibana mimi na mume wangu na kumhudumia mama,” alisema Hinju.
Hinju hayuko peke yake. Takwimu zilizotolewa na Tanzania DHS-MIS 2015-16 zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya wananchi hawana bima ya afya. Hivyo, huingia gharama kubwa katika kulipia matibabu, ikiwemo kununua dawa. Takwimu hizo zinaonyesha kuwa asilimia 89.7 wanaoishi mijini hawana bima ya afya, na asilimia 91.7 ya wanawake wanaoishi vijijini nao hawana bima ya afya. Kwa upande wa wanaume, asilimia 89.3 ya wanaume wanaoishi mijini hawana bima ya afya, wakati kwa wanaume wanaoishi vijijini ni asilimia 91.1.
Ripoti ya Twaweza, Sauti za Watu: Je, nyota njema huonekana asubuhi? (Agosti 2016), inaonyesha kuwa wananchi 6 kati ya 10 hutembelea vituo vya afya vya serikali kupata matibabu. Ripoti hiyo ya Twaweza inaeleza kuwa asilimia 61 ya wananchi hufuata matibabu kwenye vituo vya afya vya serikali. Wengine (asilimia 16) hupata matibabu kwenye vituo binafsi ama vya mashirika yasio ya kiserikali, na asilimia 13 hununua dawa madukani.
Japokuwa serikali haidhibiti bei ya dawa, bei ya dawa inatofautiana kutegemeana na umenunulia wapi. WHO inasema katika ripoti yake ya mwaka 2016, inadadavua kuwa katika vituo vya afya vya uma, ambapo wagonjwa hulipa bei kamili ya dawa, kiujumla bei za dawa zilizotengenezwa hapa na zile zilizoagizwa nje ni ghali mara 1.67 na mara 2.20 ukilinganisha na viwango vya kimataifa vya bei za dawa. Kwa wagonjwa wanaonunua dawa kwenye vituo vya watu binafsi, bei za dawa zilizotengenezwa hapa ni mara 2.01 ya viwango vya kimataifa vya bei za dawa wakati kwa dawa zilizoagizwa nje ni mara 3.01. Pia, wananchi wanayo fursa ya kutumia nyenzo iliyobuniwa na Code4Africa kuhakiki dawa waliyoinunua.
Upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya vya serikali
Ripoti ya WHO inaainisha kuwa upatikanaji wa dawa zilizotengenezwa nchini ni asilimia 21, wakati upatikanaji wa dawa zilizoagizwa kutoka nje ni asilimia 32 kwa vituo vya afya vya uma. Hata hivyo, dawa zilizotengenezwa nchini zilikuwa ghali kwa asilimia 7 kuliko zile zilizoagizwa kutoka nje ziliponunuliwa katika vituo vya serikali.
Bei za dawa zilizotengenezwa nchini zilikuwa ghali kwa asilimia 67 ukilinganisha na viwango vya kimataifa vya bei za dawa, wakati kwa dawa zilizoagizwa kutoka nje, hizo zilikuwa ghali kwa asilimia 120 kuliko viwango vya kimataifa vya bei za dawa.
Halikadhalika, serikali iliwatoza wagonjwa asilimia 135 zaidi ya bei ya manunuzi kwa dawa zilizotengenezwa nchini, na asilimia 65 kwa dawa zilizoagizwa kutoka nchi za nje.
Upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya vya watu binafsi
Hali ya upatikanaji wa dawa katika sekta binafsi, ina mlinganisho unaofanana na sekta ya uma. Upatikanaji wa dawa zailizotengenezwa nchini uko chini kwa asilimia 21, wakati dawa zilizotoka nje zinapatikana kwa asilimia 70 katika vituo vya watu binafsi. Hata hivyo, bei za dawa hazikuwa na tofauti sana kati ya zile zilizotengenezwa nchini na zilizoagizwa toka nje.
Lakini, bei za dawa zilizotengenezwa nchini zilikuwa ghali kwa asilimia 101 kuliko viwango vya kimataifa vya bei za dawa wakati dawa zilizoagizwa toka nje zilikiwa ghali kwa asilimia 201 kuliko viwango vya kimataifa vya bei za dawa.
Upatikanaji wa dawa katika vituo vya Misheni
Dawa zinazotengenezwa nchini, hupatikana kwa asilimia 18, wakati zile zinzoagizwa zikipatikana kwa wingi zaidi (asilimia 54). Tofauti inakuja katika bei. Kwani kwa vituo vya misheni, bei za dawa zilizoagizwa toka nje ni ghali kwa asilimia 47 kuliko bei ya dawa zilizotengenezwa nchini.
Utatuzi wa serikali
Tangu Raisi John Pombe Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, tumeona mabadiliko na maboresho mbalimbali yanayofanywa na serikali katika kutoa huduma za afya zenye ubora. Alipoingia tu madarakani, alifanya ziara za kushtukiza maeneo mbalimbali, ikiwepo kwenye hospitali ya Muhimbili ili ajionee mwenyewe hali ya kutoa huduma ikoje. Wadau mbalimbali walipongeza hatua hiyo, na kuzungumzia changamoto mbalimbali kwenye sekta ya afya, ikiwemo upungufu wa dawa.
Muda mfupi baada ya ziara hiyo, Raisi Magufuli aliagiza Wizara ya Afya kuhakikisha kuwa dawa na bidhaa zingine za matibabu zinanunuliwa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji badala ya kupitia kwa mawakala.
Taasisi ya Yale Global Health Leadership Institute kwenye utafiti wake imegundua kuwa “kwa wastani, kitaifa, kiasi cha dawa kinachoagizwa na kupokelewa kwenye vituo vya afya vya ngazi za chini ni asilimia 60-65.” Hii ina maana kuwa asilimia 35-40 ya dawa zinazoagizwa hazipatikani hospitalini. Mwezi Machi mwaka huu, Mkurugenzi Mkuu Bohari Kuu ya Dawa (MSD) Lauren Bwanakunu alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuwa upatikanaji wa dawa 135 muhimu uliongezeka kwa asilimia 80.
Mambo yanaanza kuwa mazuri
Ripoti ya Twaweza, pia inaonyesha mabadiliko chanya katika ongezeko la ongezeko la watumiaji wa huduma za afya za umma. Kwani kwa mwaka 2015, asilimia 47 tu ya wananchi waliripoti kutibiwa kwenye kituo cha afya cha serikali, wakati asilimia 19 walienda kwenye maduka ya dawa. Wananchi ambao hawakutibiwa kwenye vituo vya afya vya serikali walitaja sababu kuu kuwa gharama kubwa za matibabu (asilimia 43) na ugonjwa wao kutokuwa wa kuhitaji huduma ya daktari (asilimia 35). Idadi hii iliongezeka kwa mwaka 2016 kama ilivyoainishwa awali katika tathmini hii.
Wananchi 7 kati ya 10 (asilimia 70) walisema kwamba walipata baadhi ya dawa kwenye kituo cha afya, lakini wananchi 3 kati ya 10 (asilimia 28) walilazimika kwenda kununua dawa kwenye duka la dawa. Utafiti huu wa Twaweza pia unaonyesha kuwa Watu 6 kati ya 10 wanasema ukosefu wa dawa au vifaa tiba vingine kwenye vituo vya afya vya serikali ni changamoto kubwa. Asilimia 58 ya wagonjwa walitibiwa katika vituo vya afya vya serikali ndani ya miezi mitatu iliyopita. Walipoulizwa kuhusu matatizo waliyokutana nayo, asilimia 59 walitaja tatizo la
ukosefu wa dawa/vifaa tiba. Hakuna mabadiliko makubwa katika hali hii tangu mwaka 2015.
Idadi ya waliolalamikia kutokuheshimiwa na wahudumu ilishuka kutoka asilimia 42 (2015)
mpaka asilimia 27 (2016). Vilevile, ni asilimia 11 tu waliolalamikia kuwa vituo vya afya ni
vichafu, ukilinganisha na asilimia 29 mwaka 2015. Waliotaja ukosefu wa madaktari kama
changamoto walipungua kutoka asilimia 43 (2015) mpaka asilimia 18 (2016).
Dawa za kufubaza makali ya maambukizi ya virusi vya ukimwi (vvu), ARV
Dawa za ARV zina utaratibu wake. Hazipatikani hivi hivi. Serikali husambaza dawa hizi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya. Ripoti ya Sikika ya mwaka 2013 inaeleza kuwa kiasi cha 95% ya washiriki wa utafiti walioufanya, walieleza kuwa hawajawahi kukosa ARV pale walipozihitaji kwenye vituo vya afya. Asilimia 5 ya washiriki walieleza kuwa kuna wakati wamewahi kukosa kupatiwa ARV, lakini walithibitisha kuwa hiyo hutokea mara chache. Kwa mujibu wa usaili huu, washiriki hawakuona upungufu wa ARV kwani walizipata dawa hizo kama walivyoandikiwa.
Hata hivyo, tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kuna kushuka kwa utumiaji wa dawa hizi kwa makundi mbali mbali ya watu ambao wameshaanza kuzitumia. Utafiti uliochapishwa na chuo kikuu cha Mzumbe, kiliangalia sababu za hali hii kwa wanawake wajawazito wenye virusi vya ukimwi ambao kwenye jiji la Mbeya. Kikubwa kilichoonekana ni kushindwa kwa wahudumu wa afya kutoa maelekezo mazuri kuhusu umuhimu wa matumizi ya dawa hiyo..
Leave a Reply