Dar es Salaam. Tanzania ni kati ya nchi yenye kiwango kikubwa cha uzazi, ambapo tunashikilia nafasi ya 16 kati ya nchi 225. Serikali imekuwa ikijitahidi kuongeza huduma za uzazi wa mpango kote nchini. Hata hivyo, jitihada hizo zimepata mkwamo kwani bajeti ya afya imepunguzwa kwa kiasi cha asilimia 20 katika mwaka wa fedha ujao 2018/19.
Serikali ina malengo makubwa kuhusu huduma za afya ya uzazi wa mpango, kwani ililenga kuongeza bajeti ya huduma za afya ya uzazi wa mpango kutoka Sh 14 bil kwa mwaka wa fedha wa 2017/18 hadi Sh 17 bil mwaka 2020. Hata hivyo, malengo haya yako mbali na uhalisia. Shirika la Sikika, linalojikita kuwafikia vijana katika maswala ya afya ya uzazi, liliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter hivi karibuni (@Sikika1) kuwa ingawa ingawa bajeti iliyokuwa imepangwa kwaajili ya huduma za afya ya uzazi wa mpango ilikuwa ni Sh 14 bil, ni kiais cha Sh 2 bil tu kilichokuwa kimetolewa mpaka Februari 2018.
Upungufu wa bajeti ya afya unaathiri pia utoaji huduma za afya ya uzazi wa mpango kwa kiwango kikubwa. Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (National Bureau of Statistics – NBS) kwenye repoti ya Februari 2018, zinaonyesha kuwa, idadi ya watu inaongezeka kwa kasi. Ripoti hii imekadiria kuwa kutakuwa na watu milioni 54 mwaka 2018. Asilimia 44 ya idadi hii ni kundi la watoto wenye umri chini ya miaka 15.
Mathalani, kuwa na idadi kubwa ya vijana kunafanya idadi ya kiwango cha uzazi pia kiwe kikubwa. Kwa sasa, idadi ya vijana wadogo Tanzania ni mara tatu ya vijana wengine wenye umri huo huo duniani.
Ripoti ya TDHS 2015-16 inaonyesha kuwa Tanzania ina uhitaji wa huduma za afya ya uzazi wa mpango kwa asilimia 22 kwa wanawake walioolewa wenye umri kati ya miaka 15-49. Hatujaweza bado kukidhi huu uhitaji. Kwa kundi la wanawake wenye miaka 20-24, hatujakidhi uhitaji wa huduma hizi kwa asilimia 23.5.
Maamuzi ya serikali kuongeza wigo wa kuboresha huduma za afya ya uzazi wa mpango, kutoka Sh 5 bil kwenye mwaka wa fedha wa 2016/17 hadi mwaka wa fedha tuliopo, yalifanyika katika kipindi ambacho Raisi Donald Trump wa Marekani aliamua kupunguza kiwango cha fedha kinachogawaiwa na nchi hiyo katika miradi ya nchi zinazoendelea, ili kuboresha huduma za afya ya uzazi, kwa asilimia 50.
Hata hivyo, Wizara ya Afya inakadiria kuwa manunuzi ya vifaa vya uzazi wa mpango yalikuwa Sh 36 mil kwa mwaka 2017, na Sh 33 mil kwa mwaka 2018.
Akizungumza na The Citizen, Meneja Utetezi wa Shirika la Advance Family Planning (AFP), James Mlali alisema hali ya uhitaji ni kubwa kuliko kinachoingia sokoni. Asilimia 22 ya wanawake wanaohitaji huduma za afya ya uzazi wa mpango, bado hawazipati.
Mlali anasema, hali hii inachangiwa na kuisha kwa bidhaa zinazotumika, idadi ndogo ya wataalamu wa huduma za afya ya uzazi wa mpango, na kutokuwa na vituo vya afya katika maeneno ya vijijini.
Aliendelea kusema kuwa, njia ya sindano ndio inayotumika sana nchini. Njia hii huwapa wanawake hali ya usiri pale ambapo mwanaume anasita kutumia njia za afya ya uzazi wa mpango.
“Hata hivyo, sindano hazipatikani kiurahisi kwasababu ya upungufu ya watoa huduma, na upungufu wa vituo vya afya hasa kwa maeneno ya vijijini. Pia, serikali hairuhusu watoa huduma za afya ya jamii kutoa huduma ya sindano hizi,” Mlali alisema. Alieleza kuwa, vidonge vinahitaji mtumiaji awe makini kumeza kila siku na kwa wakati ulele. Pia, havina usiri. Kwa matumizi ya kondomu, wote wawili wanatakiwa kukubaliana kuitumia. Wakati mwingine, kwasababu mwanaume ana nguvu katika tamaduni zetu, mwanamke anaweza kuonewa, asisikilizwe anachotaka. Njia za uzazi wa mpango ambazo ni za kudumu, huhitaji uwepo wa mtaalamu anayeweza kuzikamilisha.
Leave a Reply