Dar es Salaam. Changamoto za kupata huduma za matibabu zipo kila mahali nchini Tanzania. Kwa kutumia nyenzo mbalimbali kama tafuta vituo vya afya , iliyotengenezwa na shirika la Code4Africa, wananchi unaweza kujua kama kuna kituo cha hudua za afya karibu yao. Hata hivyo, yapo maeneo ambayo yana matatizo kuliko mengine. Katika mikoa mitano ambayo ina uhaba wa vituo vya afya, minne ni mikoa mipya.
Takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto za mwaka 2014, ziliainisha jumla ya vituo 7,071 nchini ambavyo vinajumuisha zahanati 5,915 , vituo vya matibabu 717 , kliniki 176 na hospitali 263 .
Mkoa wa Katavi
Mkoa wa Katavi una hospitali moja tu, Hospitali ya wilaya ya Mpanda, ambayo ni sawa na asilimia moja tu ya vituo vyote vya afya mkoani humo. Kwa mujibu wa takwimu, mkoa wa Katavi una jumla ya vituo 77 vya afya ambavyo vinahudumia watu 523, 293 (Sensa 2012). Kati ya hivi, zipo zahanati 63 , vituo vya matibabu 13, na hospitali 1. Mkoa huu ulianzishwa mwaka 2012 kwa kumega mkoa wa Rukwa. Hakuna kliniki hata moja katika mkoa huu. Mkoa huu wa Katavi una vituo 46 vya kutoa huduma ya upimaji wa virusi vya ukimwi na ushauri nasaha kati ya vituo 2,672 vitoavyo huduma ya jinsi hii nchi nzima. Hii ni sawa na asilimia 1.7.
Tukilinganisha hali ilivyo mkoani Katavi na ilivyo katika mkoa wa Mbeya, tunaona tofauti kubwa. Mkoa wa Mbeya unaongoza kwa kuwa na vituo vingi vya afya nchini, ambapo vipo 471, ambayo ni sawa na asilimia 6.7. Pia mkoa huu unaongoza kwa kuwa na vituo vingi vya upimaji vvu na kutoa ushauri nasaha, ambapo vipo jumla ya vituo 317, ambayo ni sawa na asilimia 11.8.
Takwimu zinaonyesha kuwa Malaria huchangia vifo vya watoto na watu wazima mkoani Katavi kwa kiasi kikubwa. Kwa mwaka 2013, asilimia 32 ya vifo vya watoto walio na umri chini ya miaka mitano vilisababishwa na ugonjwa wa Malaria. Ugonjwa huu ulisababisha asilimia 27 ya vifo vya watu waliozidi miaka mitano.
Halikadhalika, takwimu za mwaka 2014 zinaonyesha kuwa Homa ya mapafu (Pneumonia) pamoja na Malaria vilisababisha idadi sawa ya wagonjwa waliokuwa na umri chini ya miaka mitano kulazwa hospitalini. Na kwa wagonjwa waliokuwa na umri juu ya miaka mitano, Malaria ilisababisha asilimia 48 ya vifo vyao.
Asilimia 45 ya wagonjwa walio na umri chini ya miaka mitano waliohudumiwa kwenye vituo vya afya bila kulazwa walikuwa na Malaria, kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2014. Takwimu pia zinaonyesha kuwa ilikuwa asilimia 47 kwa wagonjwa waliozidi umri wa miaka mitano.
Kwa upande wa wahudumu wa afya, takwimu zinaonyesha kuwa uwiano kati ya wahudumu wa afya na wagonjwa ni 2:2 kwa mkoa wa Katavi. Kwa mikoa yote mitano, wahudumu wa tiba ndio walio wengi, ambapo mkoani Katavi wapo 140. Huku kukiwa na wauguzi 66; afisa tabibu 31; na madaktari 7 pamoja na wahudumu wengine wa afya. Mkoani Katavi hakuna afisa wa lishe.
Mkoa wa Geita
Mkoa wa Geita ulianzishwa mwaka 2012, kwa kumega sehemu ya mikoa ya Kagera, Mwanza na Shinyanga. Mkoa huu una vituo 143 vya afya vinavyohudumia watu 1.6 milioni (Sensa 2012). Idadi hii ni chini ya asimilia kumi ya vituo vyote vya afya nchini. Katika mkoa huu, kuna zahanati 121 , vituo vya matibabu 19 , hospitali 3 huku kukiwa hamna kliniki. Mkoa huu una vituo 53 vya kutoa huduma ya upimaji wa virusi vya ukimwi na ushauri nasaha (asilimia 2).
Kama ilivyo kwa mkoa wa Katavi, takwimu za mwaka 2013 zinaonyesha kuwa ugonjwa wa Malaria ndio chanzo kikuu cha vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, ambapo husababisha asilimia 45 ya vifo. Malaria pia husababisha vifo vya watu walio na umri zaidi ya miaka mitano kwa asilimia 45.
Asilimia 60 ya wagonjwa wenye chini ya miaka mitano hulazwa kwasababu ya kuwa na Malaria, kutokana na takwimu za mwaka 2014. Wakati kwa wagonjwa waliokuwa na umri zaidi za miaka mitano, Malaria ilikuwa chanzo cha asilimia 51 ya wagonjwa kulazwa.
Halikadhalika, asilimia 54 ya wagonjwa waliokuwa na umri chini ya miaka mitano walikuwa na Malaria lakini hawakulazwa. Na asilimia 53 ya wagonjwa waliokuwa na umri zaidi ya miaka mitano, walihudumiwa bila kulazwa.
Kwa upande wa wahudumu wa afya, uwiano kati ya idadi ya wataalamu wa afya na wagonjwa ni 2:8. Mkoa wa Geita una madaktari 15 (asilimia 2); wauguzi 283 (asilimia 29); afisa tabibu 134 (asilimia 14); afisa muuguzi 6 (asilimia 0.6) na wahudumu wengine wa afya. Mkoa huu hauna Afisa Lishe.
Mkoa wa Manyara
Mkoa wa Manyara ulianzishwa mwaka 2002. Una wakazi 1.3 milioni (Sensa 2012). Kuna vituo 190 vya afya, ambavyo ni chini ya asilimia kumi ya vituo vyote vilivyoko nchini. Mkoa huu una zahanati 156 , vituo vya matibabu 22 , hospitali 10 na kliniki 2. Mkoani Manyara vipo vituo 87 vinavyotoa huduma ya upimaji vvu na ushauri nasaha (asilimia 3.3).
Takwimu za mwaka 2013 zinaonyesha kuwa Malaria huchangia vifo vya wenye umri chini ya miaka mitano kwa asilimia 19, na asilimia 14 kwa wenye umri zaidi ya miaka mitano.
Hata hivyo, takwimu za mwaka 2014 zinaonyesha kuwa asilimia 63 ya wagonjwa wenye umri chini ya miaka mitano wanaolazwa wana Malaria.
Malaria bado ni ugonjwa unaosababisha wenye umri chini ya miaka mitano kutibiwa bila kulazwa kwa wingi zaidi. Ambapo asilimia 27 kati yao wana ugonjwa huo. Kwa wagonjwa wenye umri zaidi ya miaka mitano wasiolazwa, asilimia 36 huwa na ugonjwa wa ngozi, huku wenye Malaria wakiwa ni asilimia 21.
Uwiano kati ya idadi ya wataalamu wa afya na wagonjwa ni 5. Katika mkoa huu kuna madaktari 37, wauguzi 459; afisa tiba 176 afisa lishe wawili na wahudumu wengine.
Mkoa wa Shinyanga
Mkoa wa Shinyanga una wakazi vituo 199 vya afya vinavyohudumia wakazi 1,429,342 (Sensa 2012). Kati ya hivi, 175 ni zahanati; vituo vya matibabu 17; hospitali 5 na kliniki 2. Pia, vipo vituo 91 vya kutoa huduma ya upimaji vvu na ushauri nasaha (asilimia 3.3). Asilimia 66 ya wagonjwa wenye umri chini ya miaka mitano hufa kwa ugonjwa wa Malaria. Wakati huo huchangia vifo vya wagonjwa wenye umri zaidi ya miaka mitano kwa asilimia 48, kwa takwimu za mwaka 2013. Takwimu za mwaka 2014 zinaonyesha kuwa asilimia 66 ya wagonjwa wenye umri chini ya miaka mitano waliolazwa wana Malaria. Huku wale walio na umri zaidi ya miaka mitano wakiwa ni asilimia 49.
Kwa wagonjwa ambao hawalazwi, asilimia 50 ya wagonjwa wenye umri chini ya miaka mitano huwa na Malaria. Wakati asilimia 48 ya wagonjwa wenye umri zaidi ya miaka mitano wasiolazwa huwa na Malaria. Uwiano kati ya idadi ya wataalamu wa afya na wagonjwa ni 4:4. Mkoa huu una afisa lishe mmoja tu, madaktari 15; wauguzi 431; Afisa tabibu 162 na wahudumu wengine.
Mkoa wa Simiyu
Mkoa huu ni mmoja wa mikoa mipya iliyoanzishwa mwaka 2012. Ulimegwa kutoka mkoa wa Singida, kwa upande wa Mashariki. Una wakazi 1.5 (Sensa 2012) ambao wanahudumiwa na vituo vya afya 204. Kati ya hivi, 182 ni zahanati, vituo vya matibabu 14, hospitali 5, na kliniki 3. Kwa upande wa huduma za kupima vvu na utoaji ushauri nasaha, Simiyu ina vituo 34 vinavyofanya hivyo (asilimia 1.2).
Anaemia ni chanzo kikuu cha vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano (asilimia 36), kutokana na takwimu za mwaka 2013. Ugonjwa huo huo huchangia vifo vya wenye umri zaidi ya miaka mitano kwa asilimia 19. Takwimu za mwaka 2014 zinaonyesha kuwa Malaria husababisha watu kulazwa kwa uiano ufuatao, wenye umri chini ya miaka mitano (asilimia 58); wenye umri zaidi ya miaka mitano (asilimia 49). Kwa wagonjwa wasiolzwa, takwimu zinaonyesha kuwa Malaria ni chanzo cha kwenda hospitali kupata matibabu kwa uiano ufuatao: wenye umri chini ya miaka mitano (asilimia 40); wenye umri zaidi za miaka mitano (asilimia 45).
Uwiano kati ya idadi ya wataalamu wa afya na wagonjwa ni 2:5. Hakuna bwana afya katika mkoa huu. Madaktari wapo 11; wauguzi 223; afisa tabibu 104 na wahudumu wengine.
Leave a Reply